ukubwa wa habari
26.06.2013
Rais wa Marekani, Barack Obama na familia yake wanatarajiwa kuwasili
mji mkuu wa Senegal, Dakar Jumatano usiku ili kuanza ziara ya wiki moja
katika nchi tatu za barani Afrika, ziara ambayo inalenga kuzungumzia
kuimarisha taasisi za kidemokrasia na kuchochea uwekezaji wa Marekani
barani humo. Rais anasafiri na ujumbe mkubwa wa maafisa wa uchumi wa
Marekani, wafanyabiashara na waandishi wa habari.
Rais Obama anaanza ziara yake Alhamisi kwa mazungumzo na Rais wa Senegal, Macky Sall katika makazi ya rais mjini Dakar.
Marais hao wanatarajiwa kujadili masuala ya biashara na wasi wasi wa
usalama katika eneo la Sahel barani afrika, ambalo limeona ongezeko la
harakati za wanamgambo wa kiislamu.
Uamuzi wa Obama kuitembelea Senegal, taifa dogo la Afrika magharibi
ambalo linazungumza lugha ya kifaransa, unaonekana kuunga mkono rekodi
na mwenendo wa kidemokrasia za Senegal na juhudi zake za karibuni katika
kupambana na rushwa.
Marais Obama na Sall watakuwa na mkutano wa pamoja wa waandishi wa
habari kabla ya bwana Obama kuelekea kwenye mahakama kuu ya Senegal
ambako atakuwa na maafisa wa sheria wa kieneo.
Wachambuzi wanasema Dakar ni sehemu muafaka kwa mkutano huo. Senegal
imefungua mahakama maalum ya Afrika mwaka huu kwa ajili ya kusikiliza
kesi ya rais wa zamani wa Chad, Hissene Habre kwa uhalifu dhidi ya
binadamu. Itakuwa ni mahakama ya kwanza ya Afrika kusikiliza kesi ya
kiongozi wa Afrika katika ardhi ya Afrika.
Rais Obama na familia yake alhamisi mchana watakwenda kisiwa cha Goree,
ambacho kilikuwa ni kituo cha mwisho katika biashara ya utumwa kwenye
eneo la Atlantic. Kisiwa hicho kimekuwa ni sehemu muhimu kwenda kwa
viongozi wa dunia na wamarekani wenye asili ya kiafrika.