CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimeibua madai mazito dhidi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kuwa kimepewa mamilioni ya fedha kutoka nje ya nchi, kwa nia ya kukwamisha mchakato wa Katiba Mpya.
CCM kimeibua tuhuma hizo, ikiwa ni siku chache baada ya wabunge wa upinzani kupigana ngumi na askari wa Bunge muda mfupi baada ya kupitisha hoja ya kujadili Muswada wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba.
Wabunge wa upinzani wanapinga sheria hiyo, kwa madai kuwa Zanzibar haikushirikishwa.
Akihutubia mamia ya wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika jana wilayani Kahama, Katibu wa Halmashauri Kuu, Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye, alisema kinachowasumbua Chadema hadi kufikia hatua hiyo ni mamilioni ya fedha waliyopewa kutoka nje ya nchi.
“Wenzetu hawa nasikia wamepewa mamilioni toka nje, kwa kisingizio cha kushiriki mchakato wa Katiba na kama ilivyo kwa vibaraka wengine katika bara la Afrika, lengo la fedha hizo si kuwawezesha kushiriki bali kuanzisha fujo na vurugu ili mchakato usimalizike salama kupata ajenda mwaka 2015, kwani kimsingi hawana mpya.
Nape alidai kuwa mara baada ya rasimu ya kwanza kutoka, Katibu Mkuu wao alikwenda nje ya nchi na kukaa kwa muda na kabla ya kurejea ndipo Chadema wakapanga kuanza kuzunguka na helikopta na hivyo kutaka waseme fedha hizo walikozipata.
“Walichokifanya Chadema bungeni walipanga katika mkakati wao wa 'civil disobedience' ...machafuko ya umma dhidi ya dola, mkakati ambao unaratibiwa kutoka nje na baadhi ya wale waliokuwa wakoloni katika nchi zetu za Afrika,” alisema Nape.
Naye, Katibu Mkuu wa (CCM), Abdulrahman Kinana, alisema chama hicho kimekuwa kikitumia njia ya mkato ili kutafuta madaraka ya lazima kwa Watanzania pamoja na kushindwa kuonyesha lengo katika mchakato wa uundwaji wa Katiba Mpya.
Kutokana na tuhuma hizo, gazeti hili lilimtafuta Msemaji wa Chadema, Tumaini Makene ambaye alisema imekuwa ni desturi ya CCM hasa Nape, kukituhumu chama hicho pamoja na kudai kuwa ana ushahidi wa mamilioni ya shilingi ambayo anashindwa kuthibitisha.
“Tuhuma kama hizo aliwahi kuzitoa awali, watoe ushahidi wa fedha zilikotolewa mbona anatuhumu tu? Serikali kama kiasi kikubwa cha fedha kinapitishwa na inashindwa kuchukua hatua za kudhibiti, basi ni mfu,” alisema Makene.
-Mtanzania