Ubishi
mkali ulizuka baina ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais,
Mazingira, Dk Terezya Huvisa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu
(Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi waliokuwa wakivutana juu ya
ukweli kuhusu teknolojia hiyo.
Wakati Waziri Huvisa akisema kwamba hakuna utaalamu wa aina hiyo, Lukuvi alisimamia kumpinga na kusisitiza kuwa jambo hilo lipo.
Suala
la mvua hizo lililetwa nchini na aliyekuwa Waziri Mkuu Edward Lowassa
mwaka 2007, baada ya kufanya ziara Thailand ambako alivutiwa na utaalamu
wa kutengeneza mvua na kuahidi kuuleta nchini.
Kutokana
na mvutano wa mawaziri hao, Lowassa ambaye pia ni Mbunge wa Monduli
(CCM), alipewa dakika moja na Mwenyekiti wa Bunge, Jenister Mhagama
kutoa ufafanuzi ambapo aliunga mkono hoja ya Lukuvi.
Malumbano
hayo yalisababishwa na swali la nyongeza la Mbunge wa Viti Maalumu
(Chadema), Susan Lyimo ambaye alihoji mpango wa kutengeneza mvua
ulipoishia kwa kuwa Serikali imekuwa kimya.
“Sasa
ni miaka takriban sita au saba tangu Serikali ilipokuja na mpango wa
kutengeneza mvua ambao iliuchukua kutoka nchi za wenzetu, mpango huo
umefikia wapi?” aliuliza.
Akijibu
swali hilo, Waziri Huvisa alisema: “Mimi ni Rais wa Mazingira wa
Afrika, nasema hakuna kitu kama hicho, si Marekani wala Malaysia ambao
wanaweza kutengeneza mvua, hayo ni mabadiliko ya tabianchi tu.”
Waziri
Lukuvi alionyesha kutokuridhishwa majibu hayo, ndipo aliposimama kutoa
ufafanuzi na kusema Lowassa alikwenda Thailand ambako kuna utaalamu huo
na kusisitiza kwamba upo na bado unaendelea kutumika hata Ujerumani
wanakotumia mitambo ya kijeshi kusambaratisha mawingu.
Alisema kilichokwamisha mpango huo nchini ni ufinyu wa bajeti ya Serikali.
Baada
ya majibu hayo, Lowassa alisimama akitaka kutetea wazo lake. Hata
hivyo, kabla ya kumruhusu, Mhagama alimwomba akae chini kwanza ili atoe
maelekezo.
“Mheshimiwa
Lowassa, yeye siyo waziri na hivyo hastahili kutoa majibu ya Serikali,
lakini kwa kutumia kanuni zetu bungeni kuhusu kutengeneza utaratibu
mzuri wa kuongoza Bunge, naomba Lowassa usimame sasa walau kwa dakika
moja au mbili utoe ufafanuzi,” alisema Mhagama. MWANANCHI