Wabunge
wa Kambi ya Upinzani Bungeni jana jioni walitoka ndani ya Ukumbi wa
Bunge, baada ya kupuuzwa kwa mwongozo wao wa kutaka kuahirishwa
kujadiliwa kwa Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba,
hadi hapo Zanzibar itakaposhirikishwa.Wabunge waliotoka bungeni jana
yapata saa 12.15 ni kutoka vyama vya Chadema, CUF na NCCR- Mageuzi huku
Mbunge wa Vunjo na Mwenyekiti wa Taifa wa Tanzania Labour Party (TLP,
Augustine Mrema akiendelea kubaki ukumbini
Kitendo
cha wabunge hao wa upinzani kilionekana kuwakera baadhi ya wabunge wa
CCM, ambao walisikika wakiwakejeli kwa kupiga meza huku wakisema:
"Kwendeni zenu, tumewazoea."
Wakati
wabunge hao wakiondoka, Naibu Spika wa Bunge, Job Ndugai, alikuwa
akiwasisitiza wabunge wanaobakia wawe watulivu, maana kuna usalama wa
kutosha ndani ya ukumbi huo.
"Mnaotoka nimewaona wote na mnanijua," alisikika Naibu Spika Ndugai akiwatahadharisha wabunge wa upinzani waliosusa mjadala huo.
Wabunge
wa CCM waliendeleza vituko ambapo baada ya wapinzani kutoka, wabunge
Juma Nkamia (Kondoa Kusini), Hilary Aeshi ( Sumbawanga Mjini) na Murtaza
Mangungu (Kilwa Kaskazini) walikwenda kukaa katika viti vya kambi ya
upinzani.
Kabla ya
kutoka kwa wabunge hao wabunge wawili kutoka CUF waliomba mwongozo wa
Spika, wakitaka muswada huo kuondolewa ili kuwapa nafasi Wanzanzibar
kutoa maoni yao.
Mbunge wa
Mkanyageni, Habib Mohamed Mnyaa (CUF) aliomba mwongozo akitaka muswada
huo uondolewe, hadi hapo Wazanzibar watakaposikilizwa.
Alisema
kuwa kwa maoni ya Kamati ya Katiba, Sheria na Utawala wamesikiliza maoni
ya wadau wengi, lakini Zanzibar hawakwenda kuwasikiliza wadau wa eneo
hilo.
"Na hili
suala zima katika masuala ya katiba linahitaji usawa wa washirika,
tunazungumza kitu kinachohusiana na Zanzibar na Tanzania Bara, ili
kupata maoni ya nchi nzima kuna uhalali gani wa Bunge hili kuendelea na
mjadala huu?" alihoji.
Hata
hivyo, alikatizwa na kelele za Mbunge wa Viti Maalumu, Pindi Chana
(CCM), ambaye alitoa taarifa kuwa Kamati ya Katiba, Sheria na Utawala
ilialika wajumbe mbalimbali ikiwamo Zanzibar.
"Miongoni
wa wajumbe walioalikwa ni pamoja na Mkurugenzi wa Tume ya Taifa ya
Uchaguzi ya Zanzibar pamoja na wadau mbalimbali ambao walikuja mbele ya
Katiba," alisema Pindi ambaye pia ni Mwenyekiti wa kamati hiyo.
Mbunge wa
Konde, Khatibu Said Alli (CUF), alitaka mwongozo wa Spika kuhusiana na
ujumbe mfupi wa maneno ambao aliupokea ukimtisha, kutokana na kitendo
chao cha kumuunga mkono Msemaji wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Tundu
Lissu.
"Unashabikia
mambo ya Tundu Lissu leo, endelea ila mtashughulikiwa," aliunukuu
ujumbe huo na kuongeza kuwa hafahamu umetoka kwa mbunge gani ila
wahudumu wa Bunge ndio waliompelekea.
Akijibu
mwongozo huo, Ndugai alisema kuwa ni miongoni mwa mambo ambayo
anayachukua na kuyafanyia kazi ni suala hilo. Pia Ndugai aliomba ujumbe
huo apelekewe.
"Hii ni
demokrasia mara nyingi imeshatolewa miongozo, jibu linatolewa hapo hapo
ama baadaye na kwa hoja zilizotolewa inakilazimu kiti kupata ushauri
hapo baadaye," alisema Ndugai.
Hata hivyo, baada ya Ndugai kutoa majibu hayo, wabunge wa upinzani waliamua kutoka ndani ya ukumbi huo.
Baada ya
wabunge hao kutoka Naibu Spika Ndugai aliendelea na ratiba ya Bunge kwa
kusema, jambo hilo halikupangwa kumalizika jana na kwamba litaendelea
kujadiliwa hata ikibidi hadi keshokutwa.
Hata
hivyo, Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na
Bunge), William Lukuvi, alisimama kabla ya mjadala kuendelea na kutetea
hoja kuwa makundi yote yalisikilizwa tofauti na inavyodaiwa na
wapinzani.
"Hata
katika marekebisho ya sheria mbili hizi, mimi na Mwanasheria Mkuu wa
Serikali tumekutana na viongozi wengi na mawaziri na ndiyo maana
tumeahirisha Muswada wa Sheria ya Kura ya Maoni," alisema.
Alisema,
yeye (Lukuvi) alikuwa Mwenyekiti wa ujumbe uliotumwa na Rais kuitisha
makundi ya siasa ambayo yalijadili muswada huo. Lukuvi alisema kuwa,
pande zote zimeshiriki kikamilifu katika kutoa maoni yao, "kama hizi ni
sarakasi za kisiasa mimi sijui."
Baada ya
kutoka, wabunge wa vyama vya Chadema, CUF na NCCR-Mageuzi walifanya
mkutano wa pamoja kwenye Ukumbi wa Pius Msekwa. Habari kutoka ndani ya
kikao hicho zinaeleza kuwa, wabunge hao walikubaliana kufanya kila njia
kuhakikisha wanazuia mjadala huo leo.
Pia wabunge wa CCM nao walikutana nao mara baada ya Ndugai kuahirisha kikao cha jioni.
Lissu achafua hali ya hewa
Hotuba ya
Lissu ndiyo iliyochafua hali ya hewa baada ya kuituhumu Kamati ya Bunge
ya Katiba, Sheria na Utawala kwa kutohoji watu wa Zanzibar wakati
wakikusanya maoni kuhusu muswada huo.
Alisema
licha ya kamati hiyo kukusanya maoni ya taasisi za kidini na za kiraia,
taasisi za elimu ya juu na za kitaaluma, vyama vya siasa na asasi
nyingine, lakini bado haikwenda Zanzibar kukusanya maoni ya watu wa
huko.
"Wadau
pekee walioshirikishwa kutoa maoni yao juu ya muswada huu ni Watanzania
Bara tu. Wazanzibari hawakupatiwa fursa hiyo na hawakushirikishwa
kabisa, licha ya sheria yenyewe kuwa na mambo mengi yanayoihusu
Zanzibar," alisema Lissu.
Pamoja na
suala hilo, Lissu alitaka pia Rais wa Jamhuri ya Muungano aondolewe
madaraka ya kuteua Wajumbe wa Bunge Maalumu wasiokuwa wabunge au
wawakilishi kuwa inavuruga au kuondoa kabisa dhana ya uwakilishi wa
wananchi na uhalali wa kisiasa katika mchakato wa Katiba Mpya.
Pia
alipendekeza kuongezwa kwa idadi ya wajumbe ifikie 792, kwani Tanzania
ina idadi ya watu milioni 45 kwa takwimu za Sensa ya Watu na Makazi ya
mwaka 2012.
Lissu pia
alitaka wawakilishi wa Zanzibar waongezwe bungeni, kwa Zanzibar itakuwa
na wajumbe 219 kwenye Bunge lenye wajumbe 604, sawa na takriban 36% ya
wajumbe wote. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inataka idadi iwe nusu kwa
nusu kati ya pande mbili za Muungano.
Wajumbe 166
Kutakuwa
na wajumbe 166 wasiotokana na Bunge na Baraza la Wawakilishi watateuliwa
na Rais. Kutakuwa na Wabunge 357 na Wawakilishi 81 na kufanya Bunge
Maalumu kuwa na jumla ya wajumbe 604.
Chikawe asoma muswada
Mapema
akisoma muswada huo, Waziri wa Sheria na Katiba, Mathias Chikawe alisema
Rais atakaribisha makundi mbalimbali kuwasilisha majina yasiyozidi
matatu kila kundi ambao watateuliwa kama wajumbe wa Bunge Maalumu la
Katiba. Alisema pia Kifungu cha 27 (2) kitatoa fursa kwa uhuru wa maoni
katika mijadala ya Bunge Maalumu na maoni hayo hayatahojiwa mahakamani
au sehemu yoyote nje ya Bunge Maalumu.
Chikawe
alisema Bunge Maalumu la Katiba litakaa kwa siku 70 mfululizo jijini Dar
es Salaam kwa ajili ya kujadili rasimu hiyo. Hicho kitakuwa kikao
kirefu zaidi cha Bunge kuwahi kukaa nchini Tanzania.
"Kutokana
na unyeti wa suala lenyewe muswada huo unampa nguvu Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania ya kuongeza siku 20 ili kujadili katiba," aliongeza
Chikawe.
Imeandikwa na Daniel Mjema na Sharon Sauwa