NATAKA KUISADIA MONACO IWE TISHIO BARANI ULAYA - FALCAO.
MSHAMBULIAJI nyota wa
kimataifa wa Colombia, Radamel Falcao amesema ana nia ya kuisadia klabu
ya Monaco ya Ufaransa kuwa moja ya klabu bora barani Ulaya kwa mara
nyingine tena. Akihojiwa baada ya mazoezi na timu yake ya taifa
Alhamisi, Falcao amesema anajisikia fahari Monaco kumuamini na alivutiwa
na mipango waliyokuwa nayo katika kipindi kijacho na ni mategemeo yao
kwamba wataifanikisha na kuifikisha klabu hiyo kileleni mwa mafanikio.
Akiwa Monaco nyota huyo wa zamani wa klabu ya Atletico Madrid ataungana
na winga James Rodriguez ambaye pia ni raia wa Colombia baada ya
kukubali uhamisho akitokea klabu ya FC Porto. Falcao amesema ana
mahusiano mazuri na winga huyo na sio katika soka pekee bali wamekuwa
marafiki wa karibu hata nje ya uwanja, na kummwagia sifa kwamba ni
mchezaji bora ndio maana Monaco wametumia fedha nyingi kumsajili.