MZIMU wa
kutimuliwa kwa aliyekuwa Mwakilishi wa Kiembesamaki, Mansour Yussuf
Himid (CCM), umeibukia bungeni baada ya Mbunge wa Micheweni, Haji Khatib
Kai (CUF), kudai kuwa kufukuzwa kwake ni kinyume cha Katiba ya nchi.
Kai, aliseyasema hayo jana alipokuwa akiuliza swali kwa Waziri Mkuu,
Mizengo Pinda ambapo alisema Ibara ya 18 ya Katiba imetoa uhuru kwa
mwananchi yeyote kujieleza ili mradi havunji sheria.
Kabla ya
kujibu swali hilo, Pinda alimtaka mbunge huyo kutaja jina la kiongozi
anayemzungumzi, ndipo mbunge huyo alipomtaja Mansour na kuwafanya
wabunge kuangua kicheko.
Pinda
alilijibu kwa kifupi huku akimrushia kijembe mbunge huyo kwa kusema
kwamba si jambo la ajabu mwakilishi huyo kufukuzwa mbona chama cha CUF
kilimtimua mbunge wao.
"Si ajabu
yaani kwa CCM tu, mbona nanyi chama chenu kilifanya hivyo ingawa mbunge
wenu bado ni mbunge?," alihoji Pinda kwa kifupi.
Agosti
26, mwaka huu Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (NEC) ilitangaza
kuridhia kuvuliwa uanachama kwa Mansour kama ilivyopendekezwa na
Halmashauri Kuu ya chama hicho Mkoa wa Mjini Magharibi Zanzibar.
Hatua
hiyo, ilitokana na mjumbe huyo kukabiliwa na tuhuma akidaiwa kushindwa
kusimamia malengo ya CCM na kutekeleza masharti ya uanachama. Mengine
kushindwa kutekeleza wajibu wa mwanachama na kukiuka maadili ya CCM na
Ilani ya CCM ya mwaka 2010-2015.
Agosti
18, mwaka huu Kamati ya maalumu ya Halmashauri Kuu ya CCM Zanzibar,
ilipitisha mapendekezo ya kumvua uanachama mwakilishi huyo na waziri wa
zamani wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.