KILA msanii wa muziki ndani hata nje ya nchi anakuwa na ndoto ya kupata mafanikio kutokana na kazi yake ya kimuziki anayoifanya.
Ingawa wapo baadhi ya wanamuziki nchini pia wanatamani kupata mafanikio makubwa kutokana na kazi yao ya muziki wanayoifanya, ingawa ndoto zao wengi wao zimeshindwa kufikia malengo kutokana na sababu mbalimbali.
Moja ya sababu inayosababisha ndoto kwa baadhi ya waimbaji kushindwa kufikia malengo inawezekana maslahi kuwa madogo kwenye upande wa muziki au pengine maslahi madogo kwa upande huo.
Mwanamuziki mkongwe wa muziki wa dansi nchini Muhidini Gurumo ni miongoni mwa wasanii wa kitanzania ambaye ametangaza kustaafu muziki akiwa hajapata mafanikio ya kutosha kutokana na shughuri hiyo ya muziki.
Mwanamuziki huyo ambaye hivi karibuni alitangaza kustaafu shughuri za muziki kutokana na umri wake kuwa mkubwa huku maisha yake kuwa duni kushindwa kumiliki hata baiskeli.
Kutokana na hali hiyo muimbaji huyo baada ya kutangaza kustaafu muziki wake aliamua kuunda kamati itakayomsaidia kwa kipindi alichoacha muziki ili maisha yake yaendele.
Mwanamuziki huyo ambaye ni miongoni mwa waimbaji waanzilishi wa bendi ya Msondo Ngoma, ametangaza kuacha muziki huo kutokana na umri wake kuwa mkubwa, ingawa bado anamatumaini ya muziki huo kuendelea kumlipa.
Kutokana na jambo hilo la muimbaji huyo kutangaza kustaafu muziki akiwa hana hata baskeli, kitendo hicho kilimgusa msanii wa muziki wa kizazi kipya nchini Diamond Platnum.
Ambapo hivi karibuni msanii huyo wa kizazi kipya aliamua kumpa gari muimbaji huyo kama zawadi wakati alipokuwa anazindua video yake ya wimbo wake mpya unaokwenda kwa jina la 'My Number one'.
Gari hilo alilopewa na msanii huyo inawezekana ikawa faraja kwake kwani kwa kipindi chote hicho alichoweza kukaa kwenye sanaa hiyo muimbaji huyo hakuweza kununua gari lakini mara baada ya kutangaza kustaafu ndipo alipopata zawadi ya gari hilo.
Kitendo alichofanya msanii huyo ni cha kiungwana na cha kupongezwa kwani amegundua kuwa mzee huyo anahitaji kupewa huduma kama hiyo.
Msanii huyo ameweka historia kwa mwanamuziki Gurumo kumiliki gari ambalo lilikuwa ndoto yake kwa kipindi chote alichoishi kwenye muziki, ingawa hajafanikiwa kulipata ndani ya muziki huo.
Kipindi anatangaza kustaafu muziki aliweka wazi kuwa umri wake kwa sasa umekuwa mkubwa ambapo alisema ameimba kwa kipindi cha miaka 53 akiwa jukwaani.
"Muziki ni kama asili yangu imefika wakati sasa nasema basi nawaachia vijana waweze kuendeleza muziki wetu" alisema Gurumo.Mzee huyo alianza kuimba muziki akiwa na umri wa miaka 20.
Aliweka wazi kuwa tangu aanze kuimba muziki hadi sasa ametoa kopi zaidi ya 60,000 ambazo hazijamfaidisha kimaisha hivyo ameamua kuunda kamati itakayokuwa inamsaidia katika kipindi hiki alichostaafu muziki.
Kamati hiyo iliyoundwa na Gurumo ina wanamuziki na wakurugenzi wa bendi mbalimbali akiwemo Asha Baraka, Juma Mbizo, Saidi Mdoe, Waziri Ali na Saidi Kibiriki.
HISTORIA YA GURUMO.
Amezaliwa mkoa wa Pwani wilaya ya Kisarawe 1940. Elimu ya Msingi alisoma katika Shule ya Pugu kuanzia darasa la kwanza mpaka la tatu, mwaka 1956, mjomba wake aliamua kumuamishia Dar es Salaam ambako alisoma zaidi elimu ya dini 'Kuran', Mtaa wa Lindi, Ilala.Safari yake ya muziki ilianza rasmi mnamo mwaka 1967 alipojiunga na bendi ya Nuta kabla haijabadilishwa jina na kuitwa Juwata, baadaye Ottu Jazz.
Mwaka 1978 aliamia Mlimani Park Orchestra na mwaka 1985 alijiunga na Bendi ya Orchestra Safari Sound (OSS- Ndekule) lakini siku zote maisha yake yamekuwa Msondo ambayo ndiyo bendi iliyopitia majina ya Nuta, Juwata na Ottu.
Tangu miaka ya 1960 kama ungethubutu kutamka humjui Gurumo, ungeonekana mshamba ambaye tasnia ya muziki umeipa kisogo,alikuwa staa mkubwa sana wa muziki kipindi hicho ingawa jina lake limebaki juu kuanzia nyakati hizo mpaka sasa.
Ni kamanda hodari, aliyeifanya Bendi ya Msondo ‘Msondo Ngoma’ ipate heshima kubwa mpaka ikaitwa Baba ya Muziki Tanzania. Tungo zake nyingi ni lulu ambayo haitafutika kamwe. Kinachoumiza kwa sasa ni kuona Gurumo hawezi tena kusimama jukwaani.Mzee huyo ndiye aliyeivusha Msondo kupitia majina ya Nuta, Juwata, na Ottu, ikiwa inamilikiwa na Chama cha Wafanyakazi.
Itambulike kuwa yeye akiwa na wenzake kama marehemu Shaaban Mhoja Kishiwa maarufu kama ‘TX Moshi William’, Saidi Mabera, marehemu Suleiman Mbwembwe, Othuman Momba, Joseph Maina na wengineo, ndiyo waliounganisha nguvu na kuimiliki, baada ya chama cha wafanyakazi kujiondoa katika uendeshaji wa bendi.